JELA NI MAHALI PA KUISHI KAMA SABABU YA KWENDA HUKO NI VITA DHIDI YA UONEVU, UKANDAMIZAJI WA HAKI NA UTU WA BINADAMU.
Wapendwa wapiga kura wangu na Watanzania wenzangu.
Sina wakati mgumu kuchukua maamuzi haya yanayotokea leo. Upendo huu nilio nao kwa watu wa Arusha na nchi yangu ni sababu ya msingi ya maamuzi haya. Nimetishwa mara nyingi, rafiki zangu wametishwa, jamii ya watu duni imeendelea kuishi kwa mashaka na matisho kwa muda mrefu.
Katika mazingira haya, nikawaza sana kuwa anatakiwa kutokea mtu mmoja jasiri atakayeweza kuona thamani ya watu wengine. Huyo mtu anaweza kuwa wewe lakini kwa wakati huu siwezi kumsubiri tena na nimechagua kuwa mimi nikiamini kuwa utanikuta nikiendelea na safari ya ukombozi.
Tupo wengi sana tunaotaka mabadiliko, haki na ukweli. Hata hivyo hofu, woga na mashaka yamepoteza thamani yetu yote ya maana ya kuishi.
Waliofungwa kwa kuonewa na kuteswa, waliokosa chakula na kulala nje, waliokwenda hospitali na kukosa madawa, waliokosa ajira na kipato mpaka kujikuta wametoroka familia zao, waliopoteza matumaini ya maisha, waliopora utajiri wa nchi yetu kwa manufaa yao binafsi, walionunua haki na sheria dhidi ya wajane na wanyonge na kuwapora vipato vyao vidogo na mashamba yao, USIULIZE SABABU NINI!
Nimetafakari sana na nikatambua kuwa sababu ni mimi pale nilipokuwa kimya wakati wajane na wanyonge wanaonewa.
NIliposikia wengine wanaandamana kupinga uovu, uonevu, wizi, ufisadi na ukandamizaji wa haki nikasema ni hao na wala sio mimi, kumbe nilipaswa kuwa mbele katika harakati hizi.
Nilipoona wenzangu hawawezi kupata matibabu nikasema mimi sio mgonjwa, nilipopata taarifa za rafiki zangu kufungwa kwa makosa yasiyo yao, nilipoona watoto wa mitaani wanaomba chakula, nilipoona wazee wamepoteza matumaini ya kuishi katika uzee wao, nilipoona vijana hawana ajira, nilipoona mabinti wasichana wadogo wameamua kufanya biashara ya ukahaba, NIKATAFAKARI,TENA NIKATAFAKARI, dhahabu zetu, almasi yetu, Milima na mabonde yetu, Tanzaninte yetu, samaki wetu, Uranium yetu, makaa ya mawe yetu, utalii wetu, ardhi na kilimo chetu na zaidi utu na mahusiano yetu.
Na sasa siwezi kukaa kimya tena. NI afadhali vita inayotafuta haki na usawa kuliko amani inayopumbaza na kudhalilisha utu wa mwanadamu. Na katika msingi huu hofu na mashaka vimekosa thamani kwangu, sitamwogopa mtu yoyote, mwenye silaha yoyote, mwenye cheo chochote na wala sitaogopa jela yoyote katika kupigania haki, utu wa kweli katika jamii yangu.
Wanafikiri wataendelea kutuogopesha kwa sababu wana jela na silaha, wanafikiri tutaendelea kuabudu uoga, wanafikiri wataendela kutunyanyasabila sababu ya msingi LAKINI SISI TUNAJUA TUTASHINDA KWA SABABU HAKI TUNAYOIPIGANIA NI MAKUSUDI YA MWENYEZI MUNGU.
Leo nitakwenda jela kwa hiari yangu binafsi kwa siku kadhaa na si kwa NIA YA KUJITAFUTIA UTUKUFU WANGU bali ,” JELA NI MAHALI PA KUISHI KAMA SABABU YA KWENDA HUKO NI VITA DHIDI YA UONEVU, UKANDAMIZAJI WA HAKI NA UTU WA BINADAMU.Kila mara nilipotishiwa nikagundua wanaonitishia, wananitishia kwa jela na mauti. Na mimi nikagundua na nikatambua ni afadhali kuishi miaka hamsini jela huku sababu ikiwa ni kupinga uonevu na ukandamizaji kuliko maisha ya woga na anasa yasiyo na kusudi katika kutetea utu na heshima ya mwanadamu mwenzangu.
Wale mlionitishia kunipeleka jela sasa nimetangulia kwa hiari yangu na wale mliobaki msiogope jela endeleeni kupigania ukombozi utakaoleta usawa katika nchi yenu.
Watakaotubeza na kututukana wasameheni kwani wanahitaji ukombozi wa fikra, watakaotupongeza na kutuonea huruma wafundisheni ujasiri na waambieni mapambano bado yanaendelea tunahitaji umoja wao. Nitarudi mapema. MSIOGOPE, MSIOGOPE, MSIOGOPE , MUNGU YUPO UPANDE WETU.
Mhe Godbless Lema (MB) – Arusha Mjini 31 Oktoba 2011.
No comments:
Post a Comment