Social Icons

Sikiliza Tone Radio Live Hapa, na Tembelea Website yetu www.toneradiotz.com

bre

Friday, April 1, 2011

Tafakuri Yangu Ya Leo; Kwa Watanzania Kila Siku ni Siku Ya Wajinga Si Leo Tu !

…..Kama kawaida Mungu anatupenda watanzania……
…….Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika…….

   Leo  tunapoadhimisha  siku ya wajinga duniani nimetafakari kwa kina je kwa Tanzania siku ya wajinga ni lini? kwa jinsi hali ilivyo kama watanzania tukizama kwenye fikra zetu tukawaza na kuwazua haina ubishi kuwa sisi hatuna siku maalumu ya wajinga bali kwetu ni kila uchao.
    Chukulia mfano wa hizo sentensi mbili hapo juu ya kwanza hiyo ya ….kama kawaida Mungu anatupenda watanzania….hupenda kusemwa na viongozi wetu pale wanapozungumzza mambo ya kitaifa au wakihojiwa na vyombo vya habari na sentensi ya pili hiyo ya….Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika..inatumika na waandishi wetu katika kurasa za magazeti yao na siku hizi imeanza kuwakolea viongozi wetu wakuu wanapotoa hotuba za kitaifa.
  
   Lakini hebu tufanye hesabu rahisi tu za kujumlisha na kutoa , tunaposema Mungu anatupenda tuna maana gani? Mimi nadhani viongozi wetu wanatuchezea kwa maana kuwa matatizo makubwa ya kitaifa yanayodhuru watu wanayaremba kwa msemo huo ili yawe madogo kwa maana ya kawaida tu wanapenda kutoa majibu mepesi kwa hoja nzito halikadhalika wanatoa majibu ya zamani kwa maswali mapya, Mungu alitupenda watanzania ndio maana katuumba na utajiri mkubwa wa milima, madini, ardhi nzuri, wanyama, mimea , bahari, mito na maziwa, sasa kuna haja gani ya viongozi wetu kutumia msemo huu? Bila shaka sihitaji kuuma maneno wala kupindisha ukweli wanatufanya wajinga ili watawale mtaji kidogo faida kubwa!
     Tugeukie upande wa pili wa sarafu tunaposema Mungu ibariki Tanzania tuna maana gani? Nayo ni hoja iliyo wazi kuwa Mungu ametubariki watanzania kuliko mataifa yote ulimwenguni ndio maana katupa madini ya Tanzanite ambayo hayapo popote ulimwenguni isipokuwa Tanzania pekee, ni Mungu katupa utajiri wa kila aina mito, mabonde, mabwawa, wanyama, misitu na bahari, sasa kwa haya yote sidhani kama tupo sahihi kusema Mungu ibariki Tanzania, aibariki kwa lipi tena? Vinginevyo nah ii kauli ni silaha ya ki-idelogy inayolenga kutufanya wajinga ili tutawalike kirahisi, tuikatae!
   
  Ikumbukwe kuwa wakati mwingine Mungu anachukizwa na uzembe uzembe hivyo hofu yangu ni kuwa kama tukijizoesha na upuuzi wa hizi kauli huku tukiogelea kwenye dimbwi la utajiri kuna hatari tukamuudhi Mwenyezi Mungu kisha akatuadhibu kwa maana haiingii akilini hata kidogo kwa nchi kama Tanzania kuwa na wananchi maskini na imani hata huko mbinguni malaika wanaomboleza na kulia jinsi watanzania tunavyolea umaskini wa kujitakia kabisa.
  
  Tujiulize swali rahisi tu kama kweli viongozi wetu wanadai nchi ni maskini wao mbona matajiri? Au tuhoji basi watupe mbinu za kutajirika walizotumia, nenda kamwone mwanakijiji wa kule Nyanjilinji Lindi alivyochoka kwa maisha magumu kisha mfananishe na yule mtoto wa kibosile pale Masaki anavyong’aa kwa maisha mazuri kisha ndio utabaini kuwa tunafanywa wajinga na watawala wetu kila uchao, Naam! Kwa watanzania ujinga sio leo tu bali ni kila siku!.....Tafakari!

No comments: