Social Icons

Sikiliza Tone Radio Live Hapa, na Tembelea Website yetu www.toneradiotz.com

bre

Wednesday, April 20, 2011

Taasisi zilizoendelea zaombwa kuisaidia Tanzania katika mambo ya afya



Na Anna Nkinda – Arizona
19/4/2011 Taasisi zilizoendelea ambazo zinashughulika na mambo ya afya zimeombwa kuisaidia Tanzania katika masuala ya   elimu, wataalamu wa fani ya tiba na vifaa vya afya ili nchi hiyo iweze kukabiliana na tatizo la baadhi ya vifo vinavyotokana na upungufu wa madaktari bingwa pamoja na vitendea kazi .

Ombi hilo limetolewa leo (jana) na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete wakati akiongea na wafanyakazi pamoja na wanafunzi wa Chuo kikuu cha AT Still upande wa shule ya afya ya meno na kinywa kilichopo Arizona nchini Marekani

Mama Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) alisema kuwa nchi ya Tanzania inakabiliwa na tatizo la upungufu wa wafanyakazi katika sekta ya afya  pamoja na upungufu wa vifaa katika hospitali na vituo vya afya jambo ambalo linapelekea vifo vya baadhi ya wagonjwa wakiwemo kina mama wajawazito na watoto.

“Hivi sasa vifo vya kina mama wajawazito na watoto vimepungua,  lakini bado tatizo lipo hii ni kutokana na upungufu wa vitendea kazi na wataalam mbalimbali wa Afya lakini kama mtatusaidia kutupatia ufadhili wa masomo kwa wanafunzi wa Tanzania ili waje kusoma katika chuo hiki hakika nchi itapata wataalamu wa kutosha na tatizo la madaktari bingwa litapungua kwa siku za usoni”, alisema Mama Kikwete.

Kwa upande wake  Dean of Student wa shule hiyo Jack Dillenberg alisema kuwa hivi sasa wanaangalia uwezekano wa kutoa ufadhili kwa wanafunzi mbalimbali hasa katika nchi zinazoendelea ila kitu wanachokifanya hivi sasa ni kutoa mikopo ambayo wanafunzi wanailipa taratibu mara baada ya kumaliza chuo na kupata ajira.

Dillenberg alisema,“Tutaangalia ni jinsi gani tunaweza kuwasaidia katika suala la kutoa ufadhili pamoja na madaktari bingwa ili kuweza kutatua tatizo la vifo vinavyotokana na ukosefu wa wataalamu wa fani mbalimbali za afya kwani kama vijana watasoma na kujikita zaidi katika fani ya afya hakika tatizo lililopo hivi sasa litapungua”.


Mama Kikwete yuko Arizona kwa mualiko maalum uliotolewa na Project C.U.R.E ambao wameona jitihada zake za kupambana na kuhakikisha kuwa vifo vya watoto wachanga na kina mama wajawazito vinapungua na hivyo  kuamua kufanya harambee ya kuchangia vifaa tiba kwa ajili ya hospitali, vituo vya afya na zahanati hapa nchini.
Mwisho.

No comments: