Monday, April 11, 2011
KWANINI TUNAPENDA CHIPS?
Hakuna Mmbongo utamkaribisha chips vumbi akazitolea nje, wakati mwingine wala hana haja na karibu yako, hii Tanzania bwana, wajamaa sie, binadamu wote ni ndugu kwa hivyo kama wewe unatamani chipsi vumbi na yeye atakuwa anatamani pia, hatakuwa amefanya jambo baya akivamia chips zako kabla ya karibu toka kwako.
Utafiti wa kisayansi umechapishwa katika jarida la Journal of Neuroscience. Utafiti huu unasema una uwezekano kuwa umegundua sababu ya mimi na wewe kupenda sana chakula hiki cha bei rahisi na cha haraka (fast food) japo hakina mchango wa kutosha kwa afya zetu zaidi ya kutuacha na vitambi na mashinikizo ya damu. Wanasema jibu la swali hili ni CHUMVI.
Walioendesha utafiti huu walitumia panya wa maabara na kuwaweka katika makundi mawili. Kundi la kwanza wakachomwa sindano yenye chumvi nyingi, na kundi la pili hawakupatiwa chochote. Halafu watafiti hawa wakawafanyisha panya hawa kazi zenye kuleta msongo mkubwa wa mawazo (stress). Walipokuja kupima ubongo wa panya wa makundi yote mawili wale wa waliochomwa shindano ya chumvi walionekana kuwa na msongo mdogo zaidi ya wale ambao hawakuchomwa.
Kuna uwezekano mkubwa sana watu tulio katika nchi za dunia inayoitwa ya tatu tukawa tunaguswa moja kwa moja na utafiti huu. Wengi ya watu wanaofanya kazi, hasa za kuajiriwa, wanao msongo mkubwa sana wa mawazo, na wengi wetu huku maofisini hatuna chakula kingine tunachokila kwa wingi kama chips vumbi. Huenda chumvi ndio inayotusaidia kupambana na karaha za mabosi wetu, wivu wa kipumbavu wa wenzi wetu, matusi ya makonda kwenye daladala, habari mbayambaya kila siku kwenye magazeti, televisheni, na hata intaneti. Tunajikuta tukihitaji 'chumvi yenye chips' ili kupambana na misongo hii ya mawazo inayotuzunguka.
Lakini watafiti hawa pia wanasema raha au nafuu kwenye ubongo wako ni moja tu ya sababu inayokufanya upende chips ambazo zinakuwa na chumvi (wanachosema hapa ni kwamba unapenda chumvi na sio chips, lol!).
Hebu leo jaribu kula chips bila chumvi halafu uone kama utazipenda. Kuna hatari kubwa kwamba tunakula chumvi kupindukia, na haishangazi kwa nini leo katika jamii yangu na yako tunao watu wengi wenye umri mdogo ambao wanaugua magonjwa makubwa kama shinikizo la damu. Tutazame upya lishe yetu.
Siku njema habari kwa hsani ya fotobaraza
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment