Social Icons

Sikiliza Tone Radio Live Hapa, na Tembelea Website yetu www.toneradiotz.com

bre

Friday, March 18, 2011

Wabunge wapinga bajeti ya 2011/12

Raymond Kaminyoge na Fidelis Butahe
BAADHI ya wabunge wamepinga mapendekezo ya bajeti ya Serikali ya mwaka 2011/12 inayofikia Sh 12 trilioni kwa madai haikuzingatia  kuweka vipaumbele katika maeneo muhimu kwa maendeleo ya wananchi.
Wabunge hao walisema jana kuwa vipaumbele 12 kwenye bajeti hiyo ni vingi kupita kiasi na hiyo inaashiria Serikali haikuzingatia dhamira ya kweli katika kumaliza matatizo ya wananchi.
Mapendekezo hayo ya matayarisho ya bajeti yaliwasilishwa jana na Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkulo kwenye semina ya wabunge inayoendelea jijini Dar es Salaam.Mbunge wa Bariadi Mashariki, Andrew Chenge alisema vipaumbele vilivyowekwa na Serikali ni vingi mno na haviwezi kutekelezeka.

“ Kama tuna dhamira ya kweli, tuchague vipaumbele vichache ambavyo tutakuwa na uwezo wa kuvitengea fedha,” alisema Chenge.Aliongeza kuwa ni ndoto kupata maendeleo ikiwa vitachukuliwa vipaumbele vyote kwa kuwa bajeti haitoshi.Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema), alisema kuongezeka kwa deni kwa asilimia 18 maana yake ni kwamba kila Mtanzania anadaiwa Dola za Marekani 273 jambo ambalo ni hatari kwa taifa.
“Labda tuelezwe wazi kwamba deni hili tunadaiwa na nani na tumekopa lini,” alihoji Lissu.Alisema licha ya Serikali kuweka elimu kuwa kipaumbele cha kwanza, taarifa ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda aliyoitoa bungeni mwaka jana ilionyesha kuwa Serikali imetumia Sh 55 bilioni kuboresha elimu, lakini katika mpango huo fedha zinazoonekana kutumika ni Sh 35 bilioni tu, huku akihoji fedha nyingine zimekwenda wapi.
Mbunge wa Ilala, Mussa Azzan Zungu alisema tatizo linaloikabili Serikali ni utekelezaji  na kuongeza kuwa nchi kama Swaziland imeiga mambo mengi kutoka Tanzania, lakini yenyewe iko mbele kimaendeleo.“Hivi vipaumbele inabidi vipunguzwe na kuchukuliwa vile vyenye umuhimu ili tuweze kupiga maendeleo kwa kasi, hivyo vipaumbele vingine vitakuja kuwapo wakati mwafaka,”alisema Zungu.
Aliongeza, “Hata hili suala la Kilimo Kwanza, huu ni mradi wa watu tu, suala la kilimo tatizo sio mvua ni miundombinu ya umwagiliaji, hauwezi kufanikiwa kwa sababu kuna watendaji wenye roho mbaya wanaofikiria Power Tiller tu.”
Mbunge wa Wawi, Hamad Rashid (CUF), alisema kuwa inasikitisha kuona deni la taifa linazidi kuongezeka  huku Serikali ikizidi kukopa na kuongeza kuwa fedha zinazopatikana hazitumiki ipasavyo katika shughuli za maendeleo.
“Rais ameagiza wastaafu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki walipwe, lakini hatujaona mchanganuo katika makadirio ya bajeti,  nafikiri tungekuwa na vipaumbele kama vinne au sita kwanza,” alisema Hamad.
Awali akisoma makadirio hayo, Mkulo alisema kati ya fedha hizo, matumizi ya kawaida yatakuwa Sh7.3 trilioni wakati ya maendeleo ni Sh4.5 trilioni.Mkulo alisema vipaumbele katika bajeti hiyo ni elimu, kilimo, nishati, miundombinu, viwanda na afya.Alitaja vipaumbele vingine kuwa ni maji, ardhi, rasilimali watu, sayansi na teknolojia, huduma za fedha na masuala mtambuka.
Mkulo alisema wakati Serikali inatarajia kutumia kiasi hicho cha fedha, inadaiwa dola za Marekani trilioni 11, likiwa ni ongezeko la asilimia 18. Mwaka juzi Tanzania ilikuwa inadaiwa Sh.9.3 trilioni.Alisema katika mwaka 2011/12 matarajio ya awali ni kukusanya Sh 11.9 trilioni ikilinganishwa na matarajio ya kukusanya Sh11 trilioni mwaka 2010/11.
“ Ili kuhakikisha mpango wa bajeti wa serikali kwa mwaka 2011/12  utatekelezwa ipasavyo, Serikali imedhamiria kuboresha mfumo wa ukusanyaji mapato,” alisema Mkulo.Alisema Serikali itachukua hatua za kuziba mianya ya ukwepaji kodi , kupunguza misamaha ya kodi na kutafuta vyanzo mbadala vya kugharimia miradi ya maendeleo.
Mkulo alisema pia Serikali itahakikisha inasimamia na kudhibiti usimamizi wa fedha za umma.
“Ununuzi wa magari, uendeshaji wa semina na makongamano utaendelea kufanyika kwa kibali kutoka kwa Waziri Mkuu,” alisema Mkulo.
Chanzo Mwananchi

No comments: