Wauguzi pamoja na madaktari wakiendelea kuwahudumia majeruhi
Watu 37
wamenusurika kifo baada ya basi la abiria lenye namba za usajili T 281 ARR aina
ya Scania linalofanya safari zake kati ya Mbeya na Dar es Salaam linalomilikiwa
na Kampuni ya Happy Nation kuacha
njia na kupinduka eneo la Meta Kata ya Igurusi wilaya ya Mbarali Mkoani Mbeya.
Kamanda wa
Polisi Mkoa wa Mbeya Ahmed Msangi amesema ajali hiyo imetokea leo majira ya saa
moja asubuhi basi hilo likitokea
Mbeya baada ya kupasuka gurudumu la mbele kulia kisha kupoteza uelekeo na baadaye kumgonga mpanda baiskeli na
kupinduka.
Msangi
amesema baada ya ajali hiyo Dereva wa basi hilo aliyefahamika kwa jina moja la
Shabani alikimbia ambapo Jeshi la Polisi linafanya juhudi za kumtafuta ili
kueleza sababu za ajali hiyo.
Aidha Msangi
amesema katika ajali hiyo kulikuwa na majeruhi 37 wanaume 26 wanawake 10 na
mtoto mmoja wa kiume.
Baada ya
ajali hiyo majeruhi walikimbizwa katika Hospitali ya Misheni ya Chimala ambapo
mjeruhi 10 bado wamelazwa na wanne wamekimbizwa katika Hospitali ya Rufaa Mbeya
kwa matibabu zaidi.
Kwa mujibu
wa Daktari Mkuu Mahenge wa Hospitali ya Chimala amesema kuwa waliolazwa
Hospitalini hapo ni wanaume sita na wanawake wanne na walohamishiwa Rufaa ni
wanaume wanne.
Daktari
Mahenge amesema kuwa hali za majeruhi 10 walipo Chimala hali zao zinaendelea
vema ingawa wanakabiliwa na upungufu wa damu na wameomba msaada katika kitengo
cha benki ya Damu salama Mbeya.
Hata hivyo
baadhi ya abiria wamelalamikia mwendo kasi wa basi hilo kwani baada ya kutoka
kituo kikuu cha Mabasi lilianza kwenda kwa mwendo wa kasi na mara kadhaa
walikuwa wakimuonya Dereva lakini alikuwa akikaidi.
Pia walikuwa
wakifukazana na mabasi mengine yaliyotokea Mbeya kuelekea Jijini Dar es Salaam
hali iliyosababisha basi hilo kupasuka gurudumu la kulia likiwa katika mwendo
kasi na kona kali kisha kupinduka.
Wakati huo
huo Kamanda Ahmed Msangi amesema
watu wawili wamefariki dunia wilayani Mbozi baada ya roli la mizigo
kugongana uso kwa uso na gari linalomilikwa na NSSF.
Msangi
amesema bado majina ya waliofariki hayajapatikana na kwamba Jeshi la Polisi
linafanya uchunguzi ili kubaini chanzo cha ajali na miili ya marehemu
imehifadhiwa katika Hospitali ya Serikali Mbozi.
Na Mbeya yetu
|
2 comments:
Mbeya ajali zimekuwa kama maji ya kunywa kumbe hatushangai sana. Maana madereva wameamua kutoa roho za watu mpaka wamalize maisha ya watu wote nchini. Mungu awapumzishe kwa amani walifariki na majeruhi waendelee vema mahospitalini hatimaye warudi nyumbani kuendelea na shughuli zao.
Madereva wengine ni wavuta bangi na madawa ya kulevywa.
Post a Comment