KANISA la Morovian Jimbo la Kusini
Magharibi lenye makao makuu Mkoani Mbeya limeingia katika mgawanyiko mkubwa
baada ya viongozi, Wachungaji na Waumini kutoelewa kutokana na kuvuliwa uongozi
kwa aliyekuwa Mwenyekiti wa Jimbo hilo.
Mwenyekiti aliyesimamishwa uongozi ni
Mchungaji Nosigwe Buya ambapo baadhi ya Watumishi, Waumini na Wachungaji wa
Kanisa hilo kupinga maamuzi ya kuondolewa kwa Mwenyekiti kwa madai kuwa maamuzi
hayo yalikiuka katiba ya katika.
Kutokana na kuwepo kwa mtafaruku ndani
ya kanisa hilo, Baadhi ya Wachungaji wapatao 25 wa kanisa hilo walijitokeza
mbele ya vyombo vya habari wakitoa tamko kali la kuutaka kurejeshewa kwa
madaraka yake Mwenyekiti huyo ili kunusuru kuvunjika kwa kanisa.
Wachungaji hao ambao walimchagua
Mchungaji Chilale Edward Simoni kuwa Mwenyekiti wao na Daudi Mwiligumo kusoma
tamko waliloliandaa linalopinga maamuzi ya kusimamishwa uongozi Mwenyekiti wao
wa Jimbo na kuitaka Mahakama kuingilia kati.
Akisoma tamko hilo, Mchungaji Mwiligumo
alisema jambo wanalopingana nalo ni pamoja na kikao cha kumsimamisha
Mwenyekiti kilivunja katiba ya kanisa iliyosahihishwa na kusanifiwa mwaka 2012
ibara ya 11 kifungu cha 4(iv).
Alisema kifungu hicho kinasema
Mwenyekiti asipokuwepo, Makamu mwenyekiti atakuwa mbadala yake na ibara ya 35
inasema wakati wowote Mwenyekiti asipokuwepo Makamu atakuwa Mwenyekiti lakini
katika kikao kilichomuondoa Mwenyekiti wao hata Makamu hakuwepo hivyo kikao
kilikosa uongozi.
Aliongeza kuwa katika kikao
kilichofanyika Julai 31, Mwaka jana kilimuondoa Katibu Mkuu ambaye kwa mujibu
wa Katiba ibara ya 36(2)(ii) ambacho kinataja moja ya kazi za katibu ni
kuandika Muhtasari wa kikao hivyo kikao hicho hakikua halali kutokana na
watendaji wakuu kutokuwepo.
Tamko hilo liliendelea kudai katiba ya
kanisa hilo iliendelea kuvunjwa baada ya Muumini wa kawaida aliyetajwa kwa jina
la Charles Mwakipesile kukalia kiti kinyume cha ibara ya 10(2)C ambacho
kinasema Mwenyekiti na makamu sharti wawe wachungaji.
Walisema kwa mujibu wa katiba
mwenyejukumu la kumuondoa kiongozi yeyote katika nafasi yake ni Mkutano mkuu wa
Sinodi unaohusisha wajumbe wengi na kwamba Mwenyekiti aliyeondolewa
alichaguliwa kihalali na Sinodi mwaka 2012.
Mbali na hilo wachungaji hao walidai
vipengere vingine kukiukwa ni pamoja na kumdalisha kazi Mwenyekiti huyo kinyume
na utaratibu ikiwa ni pamoja na kumpangia katika kituo kipya cha kazi ambayo ni
ya chini kuliko wadhifa aliyokuwa nao.
Pia walipinga kitendo cha Kutakiwa
Mwenyekiti huyo kuhama katika nyumba za kanisa hadi kufikia Februari 7, Mwaka
huu kinyume cha utaratibu uliwekwa na kanisa hiloambao kila kiongozi wa Kamati
tendaji hutakiwa kuishi katika nyumba zilizo ndani ya Makao makuu ya Jimbo.
Waliongeza kuwa juhudi zao zote ni
kutaka kulinusuru kanisa na kuiomba Mahakama na vyombo vya Dola kuingilia kati
kwa kumtambua Mwenyekiti wa Jimbo Mchungaji Buya kuwa ndiye Mwenyekiti halali
wa Jimbo na kuiamuru Halmashauri ya jimbo na kamati tendaji pamoja na Askofu
Alinikisa Cheyo kuitisha Mkutano wa Sinodi haraka kwa ajili ya maamuzi.
Aidha mgogoro unaoendelea ndani ya
kanisa hilo pia umemhusisha moja kwa moja Askofu wa jimbo hilo, Alinikisa Cheyo
na kwamba kuna watu wachache wanataka kulitumia kanisa kama taasisi binafsi
kujinufaisha wao wenyewe.
Kwa upande wake Askofu wa Kanisa hilo
ambaye yuko safarini Nchini Kenya, Alinikisa Cheyo alipoulizwa kwa njia ya simu
kuhusiana na jambo hilo alionesha kusikitishwa na hatua ya wachungaji
kukimbilia kwenye vyombo vya habari kwa madai kuwa hilo jambo bado liko kwenye
mazungumzo.
Alisema pamoja na yeye kuhusishwa na
jambo hilo bado wachungaji pia wamekiuka katiba kutokana na kumpelekea
malalamiko ambayo hayana mihutasari ya kikao chao pamoja na sahihi za
wachungaji waliokusanyika kufanya kikao hicho.
Alisema hata jambo wanalozungumzia
linamhusu mtu mmoja ambaye ni Mwenyekiti hivyo kutumia cheo kimoja kuivura
taasisi nzima ni makosa ili hali Mwenyekiti huyo amesimamishwa tu na sio
kufukuzwa na kwamba aliyesimamishwa anao uwezo wa kukata rufaa kupinga maamuzi
hayo.
Aliongeza kuwa milango ya mazungumzo iko
wazi hivyo sio busara kwa wachungaji kutoka nje ya kanisa na kuwaeleza watu
wengine na kuongeza kuwa Sinodi wanayoshauri kuitishwa hakuna shida yoyote
kwamba muda wowote wakitaka wataitisha.
Na Mbeya yetu
|
3 comments:
Askofu yupo ambaye anauwezo wa kushauri migogoro katika jimbo. Wachungaji pia hawakua sahihi kukimbilia katika vyombo vya habari na kuomba msaada wa mahakama. Askofu Cheyo ziba ufa kabla ya kujenga ukuta
Askofu Cheyo tatua mgogoro kabla halijawa tatizo kubwa
CHEYO ULISHAURIWA MAPEMA KUUMALIZA HUO MGOGORO MAPEMA LAKINI HUKUTAKA,LEO UNAWALAUMU WACHUNGAJI ULITAKA WAENDE WAPI,KAMA UMEONA LIMEKUWA GUMU LUDI UMALIZE P
Post a Comment